Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Hawza, Ayatullah Alireza A‘rafi, katika kikao na Baraza la Muungano wa Vikundi vya Tablighi nchini kilichofanyika Jumamosi jioni katika ofisi ya Mkurugenzi wa Hawza za Kielimu alisisitiza kwamba; hali ya sasa ni tofauti kabisa na vipindi vyote vya zamani, na akasema: Katika zama hizi tunakabiliwa na hali ya kipekee ambayo haijawahi kushuhudiwa katika historia. Mabadiliko haya, ndani ya nchi na katika kiwango cha kimataifa, yana athari kubwa sana. Baada ya “Tufan al-Aqsa” na hasa baada ya matukio ya hivi karibuni, kipindi hiki kipya ni tofauti na vipindi vyote tulivyowahi kushuhudia hapo awali.
Mkurugenzi wa Hawza za Kielimu aliendelea kusema kuwa: Katika kipindi hiki, pamoja na fursa kubwa zilizotokana na Mapinduzi ya Kiislamu katika karne nyingi, pia tunakabiliwa na changamoto na vitisho visivyokuwa na mfano ambavyo vimeathiri taasisi ya dini, wanazuoni, hawza na harakati za tablighi. Vipengele hivi viwili — fursa kubwa na changamoto kubwa — vipo sambamba na vina athari kubwa katika mustakabali wa Mapinduzi ya Kiislamu.
Akirejea hali ya kimataifa, aliongeza kuwa: Leo katika ngazi ya kimataifa tunashuhudia ushirikiano wa nguvu mbalimbali, ikiwemo utawala wa Kizayuni, Marekani, Ulaya na baadhi ya nchi za Kiarabu, ambao mara nyingi wanatembea katika mwelekeo wa lengo moja. Uratibu huu wa kimataifa unaonesha kuwepo kwa vitisho na changamoto kubwa kwa Mapinduzi ya Kiislamu.
Uungaji mkono wa kipekee wa watu duniani
Aliongeza kuwa: Hata hivyo, kinaichofanya hali hii kuwa ya kipekee ni kwamba watu duniani, hasa katika nchi mbalimbali, wameonesha uungaji mkono usio na mfano kwa fikra ya Mapinduzi ya Kiislamu na mitazamo ya kidini.
Ayatullah A‘rafi, alisema kuwa: Kwa ujumla, tuko katika hatua ambayo fursa na vitisho, vyote kwa uzito wake mkubwa, vinaunda njia ya Mapinduzi ya Kiislamu, na hali hii ina umuhimu mkubwa kwa taasisi zote za kidini na za kimapinduzi, hasa hawza za kielimu.
Akirejea fursa na vitisho vinavyolikabili jamii ya Kiislamu hususan kuhusiana na Mapinduzi ya Kiislamu, alisema: Tuko katika hali ambayo tuna fursa kubwa sana lakini pia vitisho vikubwa vinavyohitaji maandalizi ili kuvishinda. Maandalizi haya yanahitaji ujasiri, elimu, fikra, busara na azma thabiti. Bila mambo haya, kusonga mbele haitawezekana.
Alisisitiza umuhimu wa mtazamo wa kielimu na kifalsafa katika kukabiliana na changamoto kubwa na kuongeza kuwa: Ni lazima tutazame kwa kina fursa na vitisho hivi. Mojawapo ya vitisho vikuu ni utawala wa utamaduni wa Magharibi.
Mapinduzi ya Kiislamu dhidi ya ustaarabu wa Magharibi
Mkurugenzi wa Hawza za Kielimu pia alirejea historia ya ustaarabu wa Magharibi na kusema: Utamaduni na ustaarabu wa Magharibi katika karne nne au tano zilizopita umeenea duniani kwa mfululizo, na Mapinduzi ya Kiislamu ndiyo pekee yaliyosimama kwa umakini dhidi yake. Leo nchi nyingi duniani zimeathiriwa na ustaarabu huo, na Mapinduzi ya Kiislamu yanapambana na mkondo huo wa kimataifa.
Alisisitiza umuhimu wa kuuelewa ustaarabu wa Magharibi kwa mtazamo wa kina na wa kihakiki, kwa kusema: Wanafunzi wa vyuo na taasisi za elimu wanapaswa kuwa na mtazamo wa kina na wa kielimu, hasa katika sayansi za kijamii na teknolojia. Ukosoaji huu unapaswa kuwa wa kimsingi na wa kielimu. Katika misikiti na vituo vya kitamaduni, maelezo yanaweza kuwa rahisi zaidi, lakini ni lazima tuelewe kuwa ustaarabu wa Magharibi, kwa falsafa, uchumi na sayansi yake, unaathiri sana mifumo ya elimu duniani.
Kukabiliana na vitisho vya kimataifa
Alisema pia kuwa changamoto hizi zimeongezeka baada ya Mapinduzi ya Kiislamu, kwani kabla ya mapinduzi ustaarabu wa Magharibi ulikuwa umetawala kikamilifu, lakini sasa changamoto hizo zimeonekana kwa nguvu zaidi ndani ya Iran na nchi nyingine za Kiislamu, na zinahitaji mipango sahihi ya kukabiliana nazo.
Aliongeza kuwa; lazima vitisho vitambuliwe kwa mtazamo wa kielimu na wa kihakiki, na mikakati kamili iandaliwe ili kutumia vyema fursa za kihistoria.
Mabadiliko ya haraka ya teknolojia
Ayatullah A‘rafi alisema pia kuwa; sasa dunia inakabiliwa na changamoto nyingine inayotokana na maendeleo ya haraka ya teknolojia, hasa akili bandia na sayansi za utambuzi, ambazo zitakuwa na athari kubwa katika mifumo ya kijamii na kifalsafa.
Alisema; huwa anasoma kila usiku makala mpya kuhusu masuala haya na ana wasiwasi mkubwa juu yake, kwa sababu mabadiliko makubwa zaidi bado yako mbele, hasa katika sayansi za utambuzi zinazoweza kubadilisha mifumo ya sasa duniani.
Uwezo wa kihistoria wa taasisi za kidini
Mkurugenzi wa Hawza za Kielimu alisisitiza kuwa; taasisi ya wanazuoni na vituo vya kielimu na kidini vina uwezo wa kihistoria, na vijana wenye vipaji wapo ndani yake, lakini kunahitajika mtazamo mpya na wenye nguvu zaidi kukabiliana na mabadiliko haya.
Umuhimu wa kutazama mustakabali
Alisema pia kuwa; utafiti wa mustakabali na maandalizi kwa ajili ya mabadiliko yajayo ni muhimu sana, na kwamba juhudi zilizofanywa hadi sasa ni sehemu ndogo tu ya yale yanayohitajika.
Aliendelea kusema kuwa; Mapinduzi ya Kiislamu na Jamhuri ya Kiislamu yameleta mahitaji mapya katika uwanja wa dini na tablighi, mahitaji ambayo hayajawahi kuwepo hapo awali.
Aliongeza kuwa; katika zama za mapinduzi, changamoto za leo hazikuwepo, lakini sasa mabadiliko mapya yanaathiri sana shughuli za kidini na tablighi.
Ayatullah A‘rafi alisisitiza kuwa; tablighi hufanikiwa pale inapoungwa mkono na wananchi. Misikiti na majlisi za kidini zinapaswa kusimamiwa kwa ushiriki wa wananchi, kwa sababu nafasi ya watu katika jambo hili ni muhimu sana.
Aliongeza kuwa; katika uwanja wa tablighi, miradi mipya na ubunifu mbalimbali imeanzishwa, na ni muhimu kuunda mifumo ya tablighi inayolingana na mahitaji ya jamii na inayotegemea ushiriki wa wananchi.
Maoni yako